Madhara ya Kutumia Tishu kwa Wanawake-2
Wiki iliyopita tulianza kujadili mada hii ya madhara ya kiafya ya kutumia tishu kwa mwanamke. Leo tunaendelea kuanzia tulipoishia:
Pia zipo tishu za kisasa ambazo huwa zinakuwa kwenye pakti maalum, zikiwa na kemikali kwa ajili ya kukata harufu na majimaji yenye pafyumu. Hizi huwa na madhara zaidi kwa sababu kemikali zilizopo kwenye tishu hizo, huwa na athari kubwa kwa afya ya viungo vya uzazi.
Matumizi ya tishu, huchangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa Vaginosis, ambao husababisha mwanamke atokwe na uchafu kwenye sehemu zake za siri. Hii hutokea kwa sababu, katika njia ya haja kubwa, kuna bakteria ambao huwa hawana madhara kwa ajili ya kuulinda mfumo wa utoaji taka mwilini lakini bakteria hao wanapoingia kwenye viungo vya uzazi husababisha madhara.
Kwa kawaida, watumiaji wengi wa tishu, hujifuta kwa kutokea nyuma kuja mbele, jambo ambalo husababisha iwe rahisi kwa bakteria hao kuhamishwa kutoka njia ya haja kubwa mpaka kwenye mfumo wa uzazi na baadaye maambukizi hutokea.
Wataalamu wa afya, wanashauri kwamba, matumizi sahihi ya tishu, yanapaswa kuwa kama ifuatavyo:
-Hakikisha unanunua tishu zenye ubora uliothibitishwa, siku hizi umeibuka mchezo wa kutengeneza bidhaa feki ambazo hazina ubora unaotakiwa, zikiwemo tishu. Unaponunua tishu za kutumia, hakikisha unazingatia ubora na siyo bei.
-Badala ya kutumia tishu kujifuta (rub), unashauriwa kuzitumia kwa namna ya kama unachovya, kwa maana kwamba hujifuti kwa kusugua ngozi yako ili kuondoa hatari ya kupata michubuko.
– Epuka matumizi ya tishu zenye kemikali (wet diapers) au zenye manukato.
-Unapolazimika kutumia tishu kujisafisha (kama hakuna kabisa maji), lazima ujifute kwa mtindo wa kuanzia mbele kwenda nyuma, yaani, badala ya kuanzia kusafisha sehemu ya haja kubwa ndiyo uje kwenye viungo vya uzazi, anzia mbele kwenda nyuma. Hii itakusaidia kujikinga na kusambaza vijidudu vya magonjwa kutoka kwenye mfumo wa haja kubwa kwenda kwenye viungo vya uzazi.
Pendelea kutumia zaidi maji unapomaliza kujisaidia, iwe haja ndogo au kubwa na tishu zitumike kukausha unyevunyevu tu na siyo kuzitegemea kujisafishia kwa sababu hazina uwezo wa kuondoa uchafu wote bila kukusababishia madhara.
No comments:
Post a Comment